1 Wakati ule BWANA akaniambia, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, kisha uje kwangu huku mlimani, ukajifanyie na sanduku la mti.
2 Nami nitaandika juu ya hizo mbao maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, ulizozivunja, nawe uzitie ndani ya hilo sanduku.
3 Basi nikafanya sanduku la mti wa mshita, nikachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, nikakwea mle mlimani, na zile mbao mbili mkononi mwangu.
4 Naye akaandika juu ya mbao mfano wa maandiko ya kwanza, zile amri kumi, alizowaambia BWANA huko mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano; BWANA akanipa.
5 Basi nikageuka nikashuka kutoka mlimani, nikazitia mbao ndani ya sanduku nililofanya; nazo zimo humo kama alivyoniamuru BWANA.