17 Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume.
18 Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya BWANA, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako, yote mawili.
19 Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba;
20 mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili BWANA, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki.
21 Utakapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.
22 Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako.
23 Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri BWANA, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.