1 Na itakuwa, ukiisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi, na kuimiliki, na kukaa ndani yake;
2 twaa malimbuko ya ardhi, utakayoyavuna katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako; ukayatie katika kikapu, ukaende hata mahali pale atakapopachagua BWANA, Mungu wako, ili alikalishe jina lake huko.
3 Ukamwendee kuhani atakayekuwapo siku zile, ukamwambie, Ninakiri leo kwa BWANA, Mungu wako, ya kuwa nimeingia katika nchi BWANA aliyowaapia baba zetu ya kwamba atatupa.
4 Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya BWANA, Mungu wako.
5 Nawe ujibu, ukaseme mbele za BWANA, Mungu wako, Baba yangu alikuwa Mwarami karibu na kupotea, akashuka Misri, akakaa huko ugenini, nao ni wachache hesabu yao; akawa taifa kubwa huko, yenye nguvu na watu wengi.
6 Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito.