3 Ukamwendee kuhani atakayekuwapo siku zile, ukamwambie, Ninakiri leo kwa BWANA, Mungu wako, ya kuwa nimeingia katika nchi BWANA aliyowaapia baba zetu ya kwamba atatupa.
4 Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya BWANA, Mungu wako.
5 Nawe ujibu, ukaseme mbele za BWANA, Mungu wako, Baba yangu alikuwa Mwarami karibu na kupotea, akashuka Misri, akakaa huko ugenini, nao ni wachache hesabu yao; akawa taifa kubwa huko, yenye nguvu na watu wengi.
6 Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito.
7 Tukamlilia BWANA, Mungu wa baba zetu; BWANA akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu.
8 BWANA akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu;
9 naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali.