43 Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.
44 Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.
45 Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza;
46 nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele;
47 kwa kuwa hukumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote;
48 kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta BWANA juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.
49 BWANA atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake;