46 nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele;
47 kwa kuwa hukumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote;
48 kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta BWANA juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.
49 BWANA atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake;
50 taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana;
51 naye atakula uzao wa ng’ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng’ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza.
52 Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa BWANA, Mungu wako.