8 Tukaitwaa na nchi wakati huo, katika mikono ya hao wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ng’ambo ya Yordani, tokea bonde la Arnoni mpaka kilima cha Hermoni;
9 (na hiyo Hermoni Wasidoni huiita Sirioni, na Waamori huiita Seniri);
10 miji yote ya nchi tambarare, na Gileadi yote, na Bashani yote, mpaka Saleka na Edrei, nayo ni miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani.
11 (Kwani aliyesalia katika mabaki ya Warefai ni Ogu pekee, mfalme wa Bashani; tazama, kitanda chake kilikuwa kitanda cha chuma; kitanda hicho je! Hakiko Raba kwa wana wa Amoni? Urefu wake ulikuwa ni mikono kenda, na upana wake mikono minne, kwa mfano wa mkono wa mtu).
12 Na nchi hiyo tuliitwaa ikawa milki yetu, wakati huo; tokea Aroeri iliyo kwenye bonde la Arnoni, na nusu ya nchi ya milima ya Gileadi, na miji iliyokuwamo, niliwapa Wareubeni na Wagadi;
13 na nchi ya Gileadi iliyobaki, na Bashani yote, maana huo ufalme wa Ogu niliwapa nusu ya kabila ya Manase; nchi yote ya Argobu, nayo ndiyo Bashani yote. (Na nchi hii yaitwa nchi ya Warefai.
14 Yairi, mwana wa Manase, alitwaa nchi yote ya Argobu, hata mpaka wa Wageshuri na Wamaaka; akaziita nchi hizo Hawoth-yairi, kwa jina lake mwenyewe, hata hivi leo, maana, hizo nchi za Bashani.)