9 Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.
10 Tena itakuwa atakapokwisha BWANA, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe,
11 na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba;
12 ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa.
13 Mche BWANA, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake.
14 Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao;
15 kwani BWANA, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya BWANA, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi.