15 Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.
16 Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa BWANA, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo.
17 Nawe kama ukisema moyoni mwako, Mataifa haya ni mengi kunipita mimi; nitawatoaje katika milki yao?
18 Usiwaogope; kumbuka sana BWANA, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;
19 uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje BWANA, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya BWANA, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa.
20 Tena BWANA, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.
21 Usiingiwe na kicho kwa sababu yao; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu katikati yako, Mungu mkuu, mwenye utisho.