12 BWANA akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu.
13 Tena BWANA akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu;
14 niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao.
15 Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili.
16 Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng’ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru BWANA.
17 Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu.
18 Nikaanguka nchi mbele za BWANA siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kwa kumkasirisha.