6 Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa BWANA amewaleta kutoka nchi ya Misri;
7 na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa BWANA; kwa kuwa yeye asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia BWANA; na sisi tu nani, hata mkatunung’unikia?
8 Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo BWANA atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa BWANA asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia yeye; na sisi tu nani? Manung’uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya BWANA.
9 Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, Njoni karibu mbele ya BWANA; kwa kuwa yeye ameyasikia manung’uniko yenu.
10 Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa BWANA ukaonekana katika hilo wingu.
11 BWANA akasema na Musa, akinena,
12 Nimeyasikia manung’uniko ya wana wa Israeli; haya sema nao, ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.