11 Kwa kazi mtu mwenye kuchora mawe kama vile muhuri ichorwavyo, utavichora hivi vito viwili, sawasawa na majina ya wana wa Israeli, nawe utavitia katika vijalizo vya dhahabu.
12 Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli; naye Haruni atayachukua majina yao mbele za BWANA juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho.
13 Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu;
14 na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.
15 Nawe utafanya kifuko cha kifuani cha hukumu, kazi ya fundi stadi; utakifanya kwa kuiandama ile kazi ya hiyo naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani safi yenye kusokotwa, ndivyo utakavyokifanya.
16 Kitakuwa mraba, tena cha kukunjwa; urefu wake utakuwa shibiri moja, na upana wake shibiri moja.
17 Nawe ukijaze viweko vya vito, safu nne za vito; safu moja itakuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, hivi vitakuwa safu ya kwanza;