9 Hamtafukiza juu yake uvumba mgeni, wala sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, wala hamtamimina juu yake sadaka ya kinywaji.
10 Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa BWANA.
11 BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
12 Utakapowahesabu wana wa Israeli, kama itakavyotokea hesabu yao, ndipo watakapompa BWANA kila mtu ukombozi kwa ajili ya roho yake, hapo utakapowahesabu; ili kwamba yasiwe maradhi kati yao, hapo utakapowahesabu.
13 Nacho watakachotoa ni hiki, kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa atatoa nusu shekeli kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu; (shekeli ni gera ishirini;) nusu shekeli kwa sadaka ya BWANA.
14 Kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa tangu huyo ambaye umri wake ni miaka ishirini, au zaidi, atatoa hiyo sadaka ya BWANA.
15 Matajiri hawataleta zaidi, wala maskini hawataleta kilichopungua, katika hiyo nusu shekeli, watakapotoa hiyo sadaka ya BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.