9 Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako.
10 Akasema, Tazama, nafanya agano; mbele ya watu wangu wote nitatenda miujiza, ya namna isiyotendeka katika dunia yote, wala katika taifa lo lote; na watu wote ambao unakaa kati yao wataona kazi ya BWANA, kwa maana ni neno la kutisha nikutendalo.
11 Liangalie neno hili ninalokuamuru leo; tazama, mbele yako namtoa Mwamori, na Mkanaani, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.
12 Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.
13 Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.
14 Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa BWANA, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu.
15 Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake.