1 Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani.
2 Farao akasema, BWANA ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui BWANA, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.
3 Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu BWANA, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga.
4 Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu.
5 Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao.
6 Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema,