16 BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.
17 Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.
18 Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama.
19 Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.
20 BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi.
21 Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake.
22 Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.