11 Naye atamchinja hapo upande wa madhabahu ulioelekea kaskazini mbele za BWANA; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake juu ya madhabahu pande zote.
12 Kisha atamkata vipande vyake, pamoja na kichwa chake, na mafuta yake; kisha atavipanga vile vipande juu ya kuni zilizo juu ya madhabahu;
13 lakini matumbo yake, na miguu yake, ataosha kwa maji; na huyo kuhani atavisongeza vyote na kuviteketeza juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA.
14 Na matoleo yake atakayomtolea BWANA kuwa sadaka ya kuteketezwa, kwamba ni katika ndege, ndipo atakapoleta matoleo yake katika hua au katika makinda ya njiwa.
15 Kisha kuhani atamleta karibu na madhabahu, naye atamkongonyoa kichwa, na kumteketeza kwa moto juu ya madhabahu; na damu yake itachuruzishwa kando ya madhabahu;
16 kisha atakiondoa kile kibofu chake, pamoja na taka zake, na kukitupa kando ya madhabahu upande wa mashariki, mahali pa majivu;
17 kisha atampasua na mabawa yake, lakini asimkate vipande viwili; kisha kuhani atamteketeza juu ya madhabahu, juu ya kuni zilizo juu ya moto; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA.