Law. 17 SUV

Uchinjaji wa Wanyama

1 BWANA akamwambia Musa, akisema,

2 Sema na Haruni, na wanawe, na wana wote wa Israeli, ukawaambie; Neno hili ndilo aliloliamuru BWANA, akisema,

3 Mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli atakayechinja ng’ombe, au mwana-kondoo, au mbuzi, ndani ya marago, au atakayemchinja nje ya marago,

4 wala hamleti mlangoni pa hema ya kukutania, ili amtoe kuwa matoleo kwa BWANA mbele ya hema ya BWANA; mtu huyo atahesabiwa kuwa ana hatia ya damu; amemwaga damu; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake;

5 ili kusudi wana wa Israeli walete sadaka zao, wazichinjazo mashambani, naam, wazilete kwa BWANA, mpaka mlango wa hema ya kukutania, kwa huyo kuhani, ili wazichinje ziwe sadaka za amani kwa BWANA.

6 Naye kuhani atainyunyiza damu yake juu ya madhabahu ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania, na kuyateketeza mafuta yake, yawe harufu njema mbele za BWANA.

7 Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi.

8 Nawe utawaambia, Mtu awaye yote katika nyumba ya Israeli, au miongoni mwa wageni, wanaokaa nao, atoaye sadaka ya kuteketezwa au dhabihu,

9 wala haileti mlangoni pa hema ya kukutania, ili aisongeze kwa BWANA basi mtu huyo atatengwa na watu wake.

Katazo la Kula Damu

10 Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake.

11 Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.

12 Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu.

13 Mtu ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga.

14 Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.

15 Tena kila mtu atakayekula nyamafu, au nyama aliyeraruliwa na wanyama, kama ni mzalia, kama ni mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni; ndipo atakapokuwa safi.

16 Lakini kwamba hazifui, wala haogi mwili, ndipo atakapochukua uovu wake.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27