1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na Haruni na wanawe, ili wajitenge wenyewe na vitu vitakatifu vya wana wa Israeli ambavyo wanitakasia mimi, tena kwamba wasilinajisi jina langu takatifu; mimi ndimi BWANA.
3 Waambie, Mtu ye yote wa kizazi chenu chote katika vizazi vyenu, atakayevikaribia vile vitu vitakatifu, ambavyo wana wa Israeli wamtakasia BWANA, naye ana unajisi, mtu huyo atakatiliwa mbali asiwe mbele zangu; mimi ndimi BWANA.
4 Mtu ye yote wa kizazi cha Haruni aliye mwenye ukoma, au mwenye kisonono; yeye asile katika vitu vitakatifu, hata atakapokuwa safi. Tena mtu awaye yote atakayekinusa kitu kilicho na unajisi kwa sababu ya wafu, au mtu ambaye shahawa humtoka;
5 au mtu amgusaye mnyama atambaaye, wa kumpatia unajisi, au kwamba amgusa mtu wa kumpatia unajisi, kwa unajisi wo wote alio nao;
6 huyo mtu atakayegusa kitu cho chote namna hiyo atakuwa najisi hata jioni, naye hatakula katika vitu vitakatifu, asipooga mwili wake majini.
7 Jua likiisha kuchwa atakuwa safi; kisha baadaye atakula katika vitu vitakatifu, maana ni chakula chake.
8 Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi BWANA.
9 Basi kwa hiyo watayashika mausia yangu, wasije wakachukua dhambi kwa hayo, nao wakafa humo, wakiyanajisi; mimi ndimi BWANA niwatakasaye.
10 Mgeni awaye yote asile katika kitu kitakatifu; mgeni wa kuhani akaaye kwake, au mtumishi aliyeajiriwa, asile katika kitu kitakatifu.
11 Lakini kwamba kuhani akinunua mtu ye yote, kwa kumnunua kwa fedha zake, yeye atakula katika hicho; na hao waliozaliwa nyumbani mwake watakula katika chakula chake.
12 Na binti ya kuhani kwamba ameolewa na mgeni, asile katika sadaka ya kuinuliwa katika vitu vile vitakatifu.
13 Lakini kwamba binti ya kuhani ni mjane, au kwamba ameachwa na mumewe, wala hana mtoto, kisha amerudi na kuketi katika nyumba ya baba yake, kama vile katika ujana wake, yeye atakula katika chakula cha baba yake; lakini mgeni awaye yote asile katika chakula hicho.
14 Tena kama mtu ye yote akila katika kitu kilicho kitakatifu pasipo kukijua, ndipo ataongeza sehemu ya tano juu ya kitu hicho, na kumpa kuhani kitu hicho kitakatifu.
15 Wala wasivinajisi vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, wavisongezavyo kwa BWANA;
16 hata wakawatwika ule uovu uletao hatia, hapo walapo vitu vyao vitakatifu; kwa kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye.
17 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
18 Nena na Haruni na wanawe, na wana wa israeli wote, uwaambie, Mtu ye yote wa nyumba ya Israeli, au wa wageni walio katika Israeli, atakayetoa matoleo yake, kama ni nadhiri zao mojawapo, au kama ni sadaka yo yote ya hiari, watakayomtolea BWANA kuwa sadaka ya kuteketezwa;
19 ili mpate kukubaliwa, mtaleta mume mkamilifu, katika ng’ombe, au katika kondoo, au katika mbuzi.
20 Lakini mnyama ye yote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu.
21 Na mtu awaye yote atakayemtolea BWANA dhabihu katika sadaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng’ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema ndani yake cho chote.
22 Kipofu, au aliyevunjika mahali, au kiwete au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na kikoko, hamtamtolea BWANA wanyama hao, wala msiwasongeze kwa BWANA kwa njia ya moto juu ya madhabahu.
23 Ng’ombe, au mwana-kondoo aliye na kitu kilichozidi, au aliyepungukiwa na kitu katika vitu vya mwilini mwake, mna ruhusa kutoa kuwa sadaka ya moyo wa kupenda; lakini kwa ajili ya nadhiri hatakubaliwa.
24 Mnyama aliyeumia mapumbu yake, au kusetwa, au kuvunjwa, au kukatwa, msimtolee BWANA; wala msifanye hivi katika nchi yenu.
25 Wala msisongeze chakula cha Mungu wenu katika wanyama hao mmojawapo kitokacho mkononi mwa mgeni; kwa sababu uharibifu wao u ndani yao, wana kilema ndani yao; hawatakubaliwa kwa ajili yenu.
26 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
27 Hapo ng’ombe, au kondoo, au mbuzi, akizaliwa, atakuwa pamoja na mamaye muda wa siku saba; na siku ya nane na baadaye atakubaliwa kuwa ni sadaka ya kutolewa kwa BWANA kwa njia ya moto.
28 Tena kama ni ng’ombe, au kama ni kondoo, msimchinje huyo na mwanawe wote wawili kwa siku moja.
29 Tena mtakapomchinjia BWANA dhabihu ya shukrani, mtamchinja ili mpate kukubaliwa.
30 Italiwa siku iyo hiyo; msisaze kitu chake hata asubuhi; mimi ndimi BWANA.
31 Kwa hiyo mtayashika maagizo yangu, na kuyafanya; mimi ndimi BWANA.
32 Wala msilinajisi jina langu takatifu; lakini nitatakaswa mimi katika wana wa Israeli; mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi,
33 niliyewaleta mtoke nchi ya Misri, ili niwe Mungu wenu; mimi ndimi BWANA.