Law. 11 SUV

Vyakula Halali na Haramu

1 BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2 Neneni na wana wa Israeli, mkiwaambia, Wanyama hawa ndio wanyama wenye uhai mtakaowala, katika hayawani wote walio juu ya nchi.

3 Kila mnyama mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu ya kupasuka kati, mwenye kucheua, katika hayawani, hao ndio mtakaowala.

4 Pamoja na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.

5 Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.

6 Na sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.

7 Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu.

8 Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu.

9 Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao.

10 Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu,

11 watakuwa machukizo kwenu; msiile nyama yao, na mizoga yao itakuwa machukizo kwenu.

12 Kila asiye na mapezi wala magamba aliye ndani ya maji ni machukizo kwenu.

13 Kisha katika ndege hawa watakuwa ni machukizo kwenu; hawataliwa, ndio machukizo; tai, na furukombe, na kipungu;

14 na mwewe, na kozi kwa aina zake,

15 na kila kunguru kwa aina zake;

16 na mbuni, na kirukanjia, na dudumizi, na kipanga kwa aina zake;

17 na bundi, na mnandi, na bundi mkubwa;

18 na mumbi, na mwari, na mderi;

19 na korongo, na koikoi kwa aina zake, na hudihudi, na popo.

20 Tena vyote vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne, hivi ni machukizo kwenu.

21 Pamoja na hayo, hivi vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne ni halali kula, hao walio na miguu mirefu, ya kurukia juu ya nchi;

22 katika hao mna ruhusa kuwala; nzige kwa aina zake, na nzige kuu kwa aina zake, na panzi kwa aina zake, na parare kwa aina zake.

23 Lakini vyote vitambaavyo vyenye mabawa, vilivyo na miguu minne, ni machukizo kwenu.

Wanyama walio Haramu

24 Nanyi mtakuwa najisi kwa wanyama hao; kila atakayegusa mzoga wao atakuwa ni najisi hata jioni;

25 na mtu awaye yote atakayechukua cho chote cha mizoga yao atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni.

26 Kila mnyama aliyepasuliwa ukwato, naye hana kwato mbili, wala hacheui, huyo ni najisi kwenu; kila agusaye wanyama hao atakuwa ni najisi.

27 Tena kila mnyama aendaye kwa vitanga vyake, katika hao wanyama wote waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu; awaye yote atakayegusa mizoga yao, atakuwa ni najisi hata jioni.

28 Na huyo atakayechukua mzoga wa wanyama hao atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni; hao ni najisi kwenu

29 Tena katika vitu vile vitambaavyo, vitambaavyo juu ya nchi, hivi ni najisi kwenu; kicheche, na panya, na mjombakaka, kwa aina zake,

30 na guruguru na kenge, na mjusi na goromoe, na lumbwi.

31 Wanyama hao ndio walio najisi kwenu katika hao watambaao; awaye yote atakayewagusa, wakiisha kufa, atakuwa ni najisi hata jioni.

32 Tena kitu cho chote, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, wakiisha kufa, kitakuwa ni najisi; kwamba ni chombo cha mti, au nguo, au ngozi, au gunia, chombo cho chote kitakachoangukiwa, ambacho ni chombo cha kufanyia kazi yo yote, lazima kitiwe ndani ya maji, nacho kitakuwa ni najisi hata jioni; ndipo kitakapokuwa ni safi.

33 Na kila chombo cha udongo, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, kila kilichomo ndani yake kitakuwa ni najisi, na hicho chombo kitavunjwa.

34 Kila chakula kilichomo, ambacho ni kuliwa, hicho ambacho maji hutumiwa juu yake, kitakuwa ni najisi; na kila kinyweo ambacho ni cha kunywewa, kilichomo katika chombo kama hicho, kitakuwa ni najisi.

35 Na kila kitu kitakachoangukiwa na kipande cho chote cha mizoga yao kitakuwa najisi; kwamba ni tanuru, au meko ya vyungu, kitavunjwa vipande vipande; ni najisi vitu hivyo, navyo vitakuwa najisi kwenu.

36 Pamoja na hayo, chemchemi, au shimo, ambamo maji yakusanyika, vitakuwa ni safi; lakini hicho kitakachogusa mizoga yao kitakuwa ni najisi.

37 Na kipande cho chote cha mzoga kikiwa kimeangukia mbegu za kupandwa zitakazopandwa, zitakuwa safi.

38 Lakini kwamba hizo mbegu zilitiwa maji na cho chote cha mizoga yao kuziangukia, ni najisi kwenu.

39 Kama akifa mnyama awaye yote, ambaye mna ruhusa kumla, yeye anayeugusa mzoga wake atakuwa najisi hata jioni.

40 Na yeye atakayekula nyama ya mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; yeye atakayeuchukua mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni.

41 Na kila kitu kitambaacho juu ya nchi ni machukizo; hakitaliwa.

42 Kila aendaye kwa tumbo lake, na kila aendaye kwa miguu minne, na kila aendaye kwa miguu mingi, maana, ni vyote vyenye kutambaa vitambaavyo juu ya nchi, hamtavila, kwa kuwa ni machukizo.

43 Msifanye nafsi zenu kuwa ni chukizo kwa kitu cho chote chenye kutambaa, kitambaacho, wala msifanye nafsi zenu kuwa ni najisi kwa vitu hivyo, mkajipatia uchafu kwa hivyo.

44 Kwa kuwa mimi ni BWANA, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi.

45 Kwa kuwa mimi ni BWANA niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu.

46 Hii ndiyo sheria katika hao wanyama, na ndege, na kila kiumbe kilicho hai, kiendacho ndani ya maji, na kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi;

47 ili kupambanua kati ya hao walio najisi na hao walio safi, na kati ya kiumbe kilicho hai ambacho chaliwa, na hicho kilicho hai ambacho hakiliwi.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27