Law. 24 SUV

Taa Isiyozimika

1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

2 Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima.

3 Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu.

4 Atazitengeza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za BWANA daima.

Mikate ya Hema Takatifu

5 Nawe utatwaa unga mwembamba, na kuoka mikate kumi na miwili ya huo unga; sehemu za kumi mbili za efa, zitakuwa katika mkate mmoja.

6 Nawe iweke mistari miwili, mikate sita kwa kila mstari, juu ya hiyo meza safi, mbele za BWANA.

7 Nawe utatia ubani safi juu ya kila mstari, ili uwe ukumbusho kwa hiyo mikate, sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa moto.

8 Kila siku ya Sabato ataipanga mbele za BWANA daima; ni kwa ajili ya wana wa Israeli, agano la milele.

9 Nayo itakuwa ya Haruni na wanawe; nao wataila katika mahali patakatifu; kwa sababu kwake ni takatifu sana katika sadaka zisongezwazo kwa BWANA kwa moto, kwa amri ya milele.

Kufuru na Adhabu yake

10 Ikawa mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, ambaye babaye alikuwa Mmisri, akatokea kati ya wana wa Israeli; na huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, na Mwisraeli mmoja, wakapigana pamoja ndani ya marago;

11 kisha huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli akalikufuru hilo Jina, na kuapiza; nao wakamleta kwa Musa. Na jina la mamaye alikuwa akiitwa Shelomithi, binti ya Dibri, wa kabila ya Dani.

12 Nao wakamtia kifungoni, ili wapate kuambiwa neno litakalotoka kinywani pa BWANA.

13 Na BWANA akasema na Musa, na kumwambia,

14 Mtoe huyo aliyeapiza nje ya marago; na wale wote waliomsikia na waweke mikono yao kichwani mwake, kisha mkutano wote na wamwue kwa kumpiga kwa mawe.

15 Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu awaye yote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake.

16 Na yeye atakayelikufuru jina la BWANA hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzalia, hapo atakapolikufuru jina la BWANA atauawa.

17 Na mtu ampigaye mtu hata akafa, lazima atauawa;

18 na atakayempiga mnyama hata akafa atalipa; uhai kwa uhai.

19 Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo;

20 jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo.

21 Na mtu amwuaye mnyama atalipa; na yeye atakayemwua binadamu atauawa.

22 Mtakuwa na sheria moja tu, kwa huyo aliye mgeni, na kwa mzalia; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

23 Musa akanena na wana wa Israeli, nao wakamtoa huyo aliyeapiza nje ya marago, wakamwua kwa kumpiga kwa mawe. Wana wa Israeli wakafanya kama BWANA alivyomwagiza Musa.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27