12 Kisha Musa akanena na Haruni, na Eleazari, na Ithamari, hao wanawe waliobaki, Twaeni hiyo sadaka ya unga iliyosalia katika kafara za BWANA zilizotolewa kwa moto, mkaile pasipo kutiwa chachu, pale karibu na madhabahu; kwa kuwa ni takatifu sana;
13 nanyi mtaila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni haki yako, na haki ya wanao, katika hizo kafara zisongezwazo kwa BWANA kwa moto; kwani ni hivyo nilivyoagizwa.
14 Na kidari cha kutikiswa, na mguu wa kuinuliwa, mtavila katika mahali palipo safi; wewe, na wanao, na binti zako pamoja nawe; kwa maana vimetolewa kuwa ni haki yako, na haki ya wanao, katika zile kafara za sadaka za amani za wana wa Israeli.
15 Mguu wa kuinuliwa, na kidari cha kutikiswa, Watavileta pamoja na dhabihu zisongezwazo kwa njia ya moto, za hayo mafuta ili kuvitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; kisha vitakuwa ni vyako wewe, na vya wanao pamoja nawe, ni haki yenu milele, kama BWANA alivyoagiza.
16 Kisha Musa akamtafuta sana huyo mbuzi wa sadaka ya dhambi, naye, tazama, alikuwa amekwisha kuchomwa moto; naye akawakasirikia hao Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni, hao waliobaki, akawaambia,
17 Kwa nini hamkula hiyo sadaka ya dhambi katika mahali patakatifu, kwa kuwa ni takatifu sana, naye amewapa ninyi ili kuuchukua uovu wa mkutano, na kuwafanyia upatanisho mbele za BWANA?
18 Angalieni, hiyo damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu; iliwapasa kuila ndani ya mahali patakatifu, kama nilivyowaagiza.