15 Mguu wa kuinuliwa, na kidari cha kutikiswa, Watavileta pamoja na dhabihu zisongezwazo kwa njia ya moto, za hayo mafuta ili kuvitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; kisha vitakuwa ni vyako wewe, na vya wanao pamoja nawe, ni haki yenu milele, kama BWANA alivyoagiza.
16 Kisha Musa akamtafuta sana huyo mbuzi wa sadaka ya dhambi, naye, tazama, alikuwa amekwisha kuchomwa moto; naye akawakasirikia hao Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni, hao waliobaki, akawaambia,
17 Kwa nini hamkula hiyo sadaka ya dhambi katika mahali patakatifu, kwa kuwa ni takatifu sana, naye amewapa ninyi ili kuuchukua uovu wa mkutano, na kuwafanyia upatanisho mbele za BWANA?
18 Angalieni, hiyo damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu; iliwapasa kuila ndani ya mahali patakatifu, kama nilivyowaagiza.
19 Haruni akamwambia Musa, Angalia, hivi leo wamesongeza sadaka yao ya dhambi, na sadaka yao ya kuteketezwa, mbele za BWANA; kisha mambo kama haya yamenipata; tena kama ningalikula hiyo sadaka ya dhambi hivi leo, je! Lingekuwa ni jambo la kupendeza mbele za macho ya BWANA?
20 Naye Musa aliposikia hayo, yakampendeza.