3 Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya.
4 Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjombaye Haruni, na kuwaambia, Njoni karibu, mwachukue hawa ndugu zenu, mkawaondoe hapa mbele ya maskani, mwende nao nje ya marago.
5 Basi wakaja karibu, na kuwachukua, hali wamevaa nguo zao, wakawachukua nje ya marago; kama Musa alivyosema.
6 Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe Eleazari na Ithamari, Msiache wazi nywele za vichwani mwenu, wala msiyararue mavao yenu; ili kwamba msife, tena asiukasirikie mkutano wote; lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, na waomboleze kwa ajili ya hicho kichomo alichowasha BWANA.
7 Wala hamtatoka nje mlangoni mwa hema ya kukutania, msije mkafa; kwa sababu mafuta ya kutiwa ya BWANA ya juu yenu. Nao wakafanya kama hilo neno la Musa.
8 Kisha BWANA akanena na Haruni, na kumwambia,
9 Usinywe divai wala kileo cho chote, wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu;