1 Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2 Mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king’aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo;
3 na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na kwamba malaika yaliyo katika hilo pigo yamegeuka kuwa meupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na kuhani atamwangalia na kusema kuwa yu mwenye unajisi.
4 Na hicho kipaku king’aacho, kwamba ni cheupe katika ngozi ya mwili wake, na kuonekana kwake si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi, na malaika hayakugeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo;
5 kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limeshangaa, na pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena;