28 Na kama hicho kipaku kikishangaa pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kwamba yu safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili.
29 Tena mtu, mume au mke, akiwa na pigo juu ya kichwa, au katika ndevu zake,
30 ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, tena zikiwamo nywele za rangi ya manjano kisha nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi, maana, ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa, au wa ndevu.
31 Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, na tazama, kwamba kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba;
32 na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe,
33 ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena;
34 na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, na tazama, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa yu safi.