36 ndipo kuhani ataagiza kwamba watoe vyote vilivyomo nyumbani, mbele ya kuhani hajaingia ndani kuliangalia hilo pigo, ili kwamba vyote vilivyomo nyumbani visiwekwe kuwa unajisi; kisha baadaye kuhani ataingia ndani ya nyumba hiyo aitazame;
37 naye ataliangalia hilo pigo, na tazama, likiwa pigo limo ndani ya kuta za nyumba, nalo lina mashimo-mashimo, rangi ya majani, au mekundu, na kuonekana kuingia ndani kuliko huo ukuta;
38 ndipo kuhani atatoka katika nyumba hiyo mpaka mlangoni pa nyumba, na kuifunga hiyo nyumba muda wa siku saba;
39 siku ya saba kuhani atakwenda tena, naye ataangalia; na tazama, likiwa pigo limeenea katika kuta za nyumba;
40 ndipo kuhani atawaambia wayatoe hayo mawe, yaliyo na pigo, na kuyatupa mahali penye uchafu nje ya mji;
41 naye atafanya kwamba hiyo nyumba ikwanguwe ndani pande zote, na chokaa watakayokwangua wataimwaga nje ya mji mahali palipo na uchafu;
42 kisha watatwaa mawe mengine, na kuyatia mahali pa mawe hayo; naye atatwaa chokaa nyingine, na kuipaka chokaa hiyo nyumba.