23 Kwamba ni katika kitanda, au cho chote alichokikalia huyo mwanamke, atakapokigusa kitu hicho, atakuwa najisi hata jioni.
24 Na mtu ye yote atakayelala na mwanamke na unajisi ukawa juu yake, atakuwa najisi muda wa siku saba; na kila kitanda alichokilalia kitakuwa najisi.
25 Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo si katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatoka damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutoka damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa katika siku za kutengwa kwake; yeye yu najisi.
26 Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake.
27 Na mtu ye yote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
28 Lakini huyo mwanamke kwamba ametakaswa na kule kutoka damu kwake, ndipo atakapojihesabia siku saba, na baadaye atakuwa safi.
29 Siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania.