2 Tena uwaambie wana wa Israeli, Mtu awaye yote miongoni mwa wana wa Israeli, au miongoni mwa wageni waketio katika Israeli, atakayetoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, sharti atauawa; wenyeji wa nchi watampiga kwa mawe.
3 Mimi nami nitamkazia uso wangu mtu huyo, nami nitamkatilia mbali na watu wake; kwa kuwa ametoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, ili kupatia unajisi patakatifu pangu, na kulinajisi jina langu takatifu.
4 Tena kama wenyeji wa nchi wakimfumbia macho mtu huyo kwa njia yo yote, hapo atoapo katika kizazi chake na kumpa Moleki, wasimwue;
5 ndipo mimi nitamkazia uso wangu mtu huyo, na jamaa zake, nami nitamkatilia mbali, na hao wote wamwandamao katika uzinifu, ili kufanya uzinifu pamoja na Moleki, watengwe mbali na watu wao.
6 Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake.
7 Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
8 Nanyi zishikeni sheria zangu, na kuzitenda; Mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi.