1 Kisha BWANA akamwambia Musa, Nena na hao makuhani, wana wa Haruni, uwaambie, Mtu asijinajisi kwa ajili ya wafu katika watu wake;
2 isipokuwa ni kwa ajili ya jamaa yake wa karibu, kwa ajili ya mama yake, na kwa ajili baba yake, na kwa ajili ya mwanawe, na kwa ajili ya binti yake, na kwa ajili ya nduguye mwanamume;
3 na kwa ajili ya umbu lake aliye mwanamwali, aliye wa udugu kwake, ambaye hajaolewa na mume; ana ruhusa kujitia unajisi kwa ajili yake huyo.
4 Asijitie unajisi, ijapokuwa ni mkubwa katika watu wake, hata akajinajisi.
5 Wasijifanyie upaa kichwani, wala wasinyoe pembe za ndevu zao, wala wasichanje chale katika miili yao.
6 Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala wasilinajisi jina la Mungu wao; kwa kuwa wao ndio wasongezao sadaka za BWANA kwa njia ya moto, chakula cha Mungu wao; kwa ajili ya hayo watakuwa watakatifu.
7 Wasimwoe mwanamke aliye kahaba, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake.