13 Lakini kwamba binti ya kuhani ni mjane, au kwamba ameachwa na mumewe, wala hana mtoto, kisha amerudi na kuketi katika nyumba ya baba yake, kama vile katika ujana wake, yeye atakula katika chakula cha baba yake; lakini mgeni awaye yote asile katika chakula hicho.
14 Tena kama mtu ye yote akila katika kitu kilicho kitakatifu pasipo kukijua, ndipo ataongeza sehemu ya tano juu ya kitu hicho, na kumpa kuhani kitu hicho kitakatifu.
15 Wala wasivinajisi vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, wavisongezavyo kwa BWANA;
16 hata wakawatwika ule uovu uletao hatia, hapo walapo vitu vyao vitakatifu; kwa kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye.
17 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
18 Nena na Haruni na wanawe, na wana wa israeli wote, uwaambie, Mtu ye yote wa nyumba ya Israeli, au wa wageni walio katika Israeli, atakayetoa matoleo yake, kama ni nadhiri zao mojawapo, au kama ni sadaka yo yote ya hiari, watakayomtolea BWANA kuwa sadaka ya kuteketezwa;
19 ili mpate kukubaliwa, mtaleta mume mkamilifu, katika ng’ombe, au katika kondoo, au katika mbuzi.