21 Na mtu awaye yote atakayemtolea BWANA dhabihu katika sadaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng’ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema ndani yake cho chote.
22 Kipofu, au aliyevunjika mahali, au kiwete au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na kikoko, hamtamtolea BWANA wanyama hao, wala msiwasongeze kwa BWANA kwa njia ya moto juu ya madhabahu.
23 Ng’ombe, au mwana-kondoo aliye na kitu kilichozidi, au aliyepungukiwa na kitu katika vitu vya mwilini mwake, mna ruhusa kutoa kuwa sadaka ya moyo wa kupenda; lakini kwa ajili ya nadhiri hatakubaliwa.
24 Mnyama aliyeumia mapumbu yake, au kusetwa, au kuvunjwa, au kukatwa, msimtolee BWANA; wala msifanye hivi katika nchi yenu.
25 Wala msisongeze chakula cha Mungu wenu katika wanyama hao mmojawapo kitokacho mkononi mwa mgeni; kwa sababu uharibifu wao u ndani yao, wana kilema ndani yao; hawatakubaliwa kwa ajili yenu.
26 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
27 Hapo ng’ombe, au kondoo, au mbuzi, akizaliwa, atakuwa pamoja na mamaye muda wa siku saba; na siku ya nane na baadaye atakubaliwa kuwa ni sadaka ya kutolewa kwa BWANA kwa njia ya moto.