13 Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini.
14 Nanyi msile mkate, wala bisi, wala masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hata mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote.
15 Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba;
16 hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka ya unga mpya.
17 Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa BWANA.
18 Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, walio wakamilifu, wa mwaka wa kwanza, na ng’ombe mume mmoja, na kondoo waume wawili; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
19 Nanyi mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani.