36 Mtamsongezea BWANA sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
37 Sikukuu za BWANA ni hizi, ambazo mtazipigia mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee BWANA sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake;
38 zaidi ya hizo Sabato za BWANA, na zaidi ya matoleo yenu, na zaidi ya hizo nadhiri zenu zote, na zaidi ya sadaka zenu za hiari, ambazo mwampa BWANA.
39 Lakini siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, hapo mtakapokuwa mmekwisha kuyachuma mavuno ya nchi, mtaweka sikukuu ya BWANA muda wa siku saba; siku ya kwanza kutakuwa na kustarehe kabisa, na siku ya nane kutakuwa na kustarehe kabisa.
40 Nanyi siku ya kwanza mtajipatia matunda ya miti mizuri, na makuti ya mitende, na matawi ya miti minene, na mierebi ya vijitoni; nanyi mtafurahi mbele za BWANA, Mungu wenu, muda wa siku saba.
41 Nanyi mtaishika kuwa sikukuu kwa BWANA muda wa siku saba katika mwaka; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; mtaishika katika mwezi wa saba.
42 Mtakaa katika vibanda muda wa siku saba; wazalia wote wa Israeli watakaa katika vibanda;