1 BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2 Mtwae Haruni, na wanawe pamoja naye, na yale mavazi, na mafuta ya kutia, na ng’ombe mume wa sadaka ya dhambi, na kondoo waume wawili, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu;
3 kisha ukutanishe mkutano wote hapo mlangoni pa hema ya kukutania.
4 Basi Musa akafanya kama alivyoambiwa na BWANA; na huo mkutano ulikutanishwa mlangoni pa hema ya kukutania.
5 Musa akawaambia mkutano, Neno aliloliagiza BWANA kwamba lifanywe, ni hili.
6 Basi Musa akawaleta Haruni na wanawe, akawaosha kwa maji.
7 Kisha akamvika Haruni ile kanzu, na kumfunga mshipi, na kumvika joho, na kumvika naivera, na kumfunga huo mshipi wa kazi ya mstadi wa naivera na kumfunga naivera kwa huo mshipi.