1 Basi ilikuwa siku ya nane, Musa akawaita Haruni na wanawe, pamoja na wazee wa Israeli;
2 akamwambia Haruni, Twaa wewe mwana-ng’ombe mume awe sadaka ya dhambi, na kondoo mume wa sadaka ya kuteketezwa, wakamilifu, ukawasongeze mbele ya BWANA.
3 Nawe utawaambia wana wa Israeli, ukisema, Twaeni mbuzi mume awe sadaka ya dhambi; na mwana-ng’ombe, na mwana-kondoo, wote wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, kwa sadaka ya kuteketezwa;
4 na ng’ombe mume, na kondoo mume, kwa sadaka za amani, ili kuwachinja mbele za BWANA; na sadaka ya unga uliochanganywa na mafuta; kwa maana, BWANA hivi leo atawatokea.
5 Nao wakayaleta hayo yaliyoagizwa na Musa wakayaweka mbele ya hema ya kukutania; kisha mkutano wote ukakaribia wakasimama mbele za BWANA.
6 Kisha Musa akasema, Neno aliloliagiza BWANA kwamba mlifanye ni hili; na huo utukufu wa BWANA utawatokea.