4 na ng’ombe mume, na kondoo mume, kwa sadaka za amani, ili kuwachinja mbele za BWANA; na sadaka ya unga uliochanganywa na mafuta; kwa maana, BWANA hivi leo atawatokea.
5 Nao wakayaleta hayo yaliyoagizwa na Musa wakayaweka mbele ya hema ya kukutania; kisha mkutano wote ukakaribia wakasimama mbele za BWANA.
6 Kisha Musa akasema, Neno aliloliagiza BWANA kwamba mlifanye ni hili; na huo utukufu wa BWANA utawatokea.
7 Musa akamwambia Haruni, Ikaribie madhabahu, uitoe sadaka yako ya dhambi, na sadaka yako ya kuteketezwa, ukafanye upatanisho kwa ajili ya nafsi yako, na kwa ajili ya watu; nawe uitoe hiyo dhabihu ya watu, ukafanye upatanisho kwa ajili yao; kama BWANA alivyoagiza.
8 Basi Haruni akakaribia madhabahuni, akamchinja huyo mwana-ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliyekuwa kwa ajili ya nafsi yake.
9 Kisha wana wa Haruni wakamsongezea Haruni ile damu; naye akatia kidole chake katika damu, na kuitia katika pembe za madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu;
10 lakini mafuta, na figo, na kitambi kilichotoka katika ini ya hiyo sadaka ya dhambi, akaviteketeza juu ya madhabahu, kama BWANA alivyomwagiza Musa.