12 Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema BWANA wa majeshi.
13 Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema BWANA. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?
14 Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za BWANA wa majeshi?
15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.
16 Ndipo wale waliomcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake.
17 Nao watakuwa wangu, asema BWANA wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye.
18 Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia.