1 Hili ndilo neno la BWANA lililomjia Mika, Mmorashti, katika siku za Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; maono aliyoyaona katika habari za Samaria, na Yerusalemu.
2 Sikilizeni, enyi watu wa kabila zote; sikiliza, Ee dunia, na vyote vilivyomo; Bwana MUNGU na ashuhudie juu yenu, yeye Bwana kutoka hekalu lake takatifu.
3 Kwa maana, angalieni, BWANA anakuja akitoka mahali pake, naye atashuka, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka.
4 Na hiyo milima itayeyuka chini yake, nayo mabonde yatapasuliwa, kama vile nta iliyo mbele ya moto, kama maji yaliyomwagika tena kutelemka gengeni.
5 Kwa sababu ya kosa la Yakobo yametokea haya yote, na kwa sababu ya makosa ya nyumba ya Israeli. Nini kosa la Yakobo? Je, silo Samaria? Na nini mahali pa Yuda palipoinuka? Sipo Yerusalemu?