Mik. 2 SUV

Maovu ya Jamii Yashutumiwa

1 Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao.

2 Nao hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake.

3 Basi BWANA asema hivi, Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya.

4 Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema,Sisi tumeangamizwa kabisa;Yeye analibadili fungu la watu wangu;Jinsi anavyoniondolea hilo!Awagawia waasi mashamba yetu.

5 Kwa hiyo hutakuwa na mtu atakayeitupa kamba kwa kura katika mkutano wa BWANA.

6 Msitabiri, ndivyo watabirivyo; wasiyatabiri mambo haya; lawama hazikomi.

7 Je! Litasemwa neno hili, enyi nyumba ya Yakobo, Roho ya BWANA imepunguzwa? Je! Haya ni matendo yake? Je! Maneno yangu hayamfai yeye aendaye kwa unyofu?

8 Lakini siku hizi mmeinuka kama adui za watu wangu; mwaipokonya joho iliyo juu ya nguo za hao wapitao salama kama watu wasiopenda vita.

9 Wanawake wa watu wangu mwawatupa nje ya nyumba zao nzuri; watoto wao wachanga mwawanyang’anya utukufu wangu milele.

10 Ondokeni, mwende zenu; maana hapa sipo mahali pa raha yenu; kwa sababu ya uchafu mtaangamizwa, naam, kwa maangamizo mazito sana.

11 Mtu akienda kwa roho ya uongo, akinena maneno ya uongo, akisema, Nitakutabiria habari ya mvinyo na kileo; mtu huyu atakuwa nabii wao watu hawa.

Ahadi kwa Mabaki wa Israeli

12 Hakika nitakukusanya, Ee Yakobo, nyote pia;Bila shaka nitawakusanya waliobaki wa Israeli;Nitawaweka pamoja kama kondoo wa Bozra;Kama kundi la kondoo kati ya malisho yao;Watafanya mvumo kwa wingi wa watu;

13 Avunjaye amekwea juu mbele yao;Wamebomoa mahali, wakapita mpaka langoni,Wakatoka nje huko;Mfalme wao naye amepita akiwatangulia,Naye BWANA ametangulia mbele yao.

Sura

1 2 3 4 5 6 7