1 Nikasema, Tafadhali sikieni, enyi vichwa vya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli. Je! Haiwapasi ninyi kujua hukumu?
2 Ninyi mnaoyachukia mema, na kuyapenda mabaya; ninyi mnaowachuna watu ngozi yao, na nyama mifupani mwao.
3 Naam, mnakula nyama ya watu wangu, na kuwachuna ngozi zao, na kuivunja mifupa yao; naam, kuwakata vipande vipande kama kwa kutiwa chunguni, na kama nyama sufuriani.
4 Ndipo watakapomwomba BWANA, asiwaitikie; naam, atawaficha uso wake wakati huo, kwa kadiri walivyotenda mabaya kwa matendo yao.
5 BWANA asema hivi katika habari za manabii wanaowakosesha watu wangu; hao waumao kwa meno yao, na kulia, Amani; na mtu awaye yote asiyetia kitu vinywani mwao, wao humwandalia vita.
6 Kwa hiyo itakuwa usiku kwenu, msipate kuona maono; tena itakuwa giza kwenu, msiweze kubashiri; nalo jua litawachwea manabii, nao mchana utakuwa mweusi juu yao.
7 Na hao waonaji watatahayarika, na wenye kubashiri watafadhaika; naam, hao wote watajifunika midomo yao; kwa maana; hapana jawabu la Mungu.
8 Bali mimi, hakika nimejaa nguvu kwa roho ya BWANA; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubiri Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake.
9 Sikieni haya, tafadhali, enyi vichwa vya nyumba ya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli, mnaochukia hukumu, na kuipotosha adili.
10 Wanaijenga Sayuni kwa damu, na Yerusalemu kwa uovu.
11 Wakuu wake huhukumu ili wapate rushwa, na makuhani wake hufundisha ili wapate ijara, na manabii wake hubashiri ili wapate fedha; ila hata hivyo watamtegemea BWANA, na kusema, Je! Hayupo BWANA katikati yetu? Hapana neno baya lo lote litakalotufikia.
12 Basi, kwa ajili yenu, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu; na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni.