3 Naye atafanya hukumu kati ya watu wa kabila nyingi, naye atawakemea mataifa wenye nguvu walio mbali; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.
4 Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.
5 Kwa maana mataifa yote watakwenda, kila moja kwa jina la mungu wake, na sisi tutakwenda kwa jina la BWANA, Mungu wetu, milele na milele.
6 Katika siku ile, asema BWANA, nitamkusanya yeye achechemeaye, nami nitamrudisha yeye aliyefukuzwa, na yeye niliyemtesa.
7 Nami nitamfanya yeye aliyechechemea kuwa mabaki, na yeye aliyetupwa mbali kuwa taifa lenye nguvu, na BWANA atawamiliki katika mlima Sayuni tangu sasa na hata milele.
8 Na wewe, Ee mnara wa kundi, kilima cha binti Sayuni, utajiliwa; naam, mamlaka ya kwanza yatakuja, ufalme wa binti Yerusalemu.
9 Sasa mbona unapiga kelele? Je! Hakuna mfalme kwako, mshauri wako amepotea, hata umeshikwa na utungu kama mwanamke wakati wa kuzaa?