11 Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao.
12 Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.
13 Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA.
14 BWANA akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi;
15 maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.
16 Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako nao utahesabika.
17 Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo.