1 Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi.
2 Akasema, Bwana zangu, karibuni nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu, hata asubuhi mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku kucha.
3 Akawasihi sana, nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia karamu, akawapikia mikate isiyochachwa nao wakala.
4 Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote.
5 Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua.