1 Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari.
2 BWANA akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia.
3 Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.
4 Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia.