1 Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko.
2 BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.
3 Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake.
4 Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake.
5 Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.
6 Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu.Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri.
7 Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami.