14 Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao.
15 Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.
16 Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani.
17 Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto;
18 na tazama, ng’ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini.
19 Kisha, tazama, ng’ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu.
20 Na hao ng’ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng’ombe saba wa kwanza, wale wanono.