1 Enyi nyumba ya Israeli, lisikieni neno awaambialo BWANA;
2 BWANA asema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni; maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo.
3 Maana desturi za watu hao ni ubatili, maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka.
4 Huupamba kwa fedha na dhahabu; huukaza kwa misumari na nyundo, usitikisike.
5 Mfano wao ni mfano wa mtende, kazi ya cherehani, hawasemi; hawana budi kuchukuliwa, kwa sababu hawawezi kwenda. Usiwaogope; kwa maana hawawezi kutenda uovu, wala hawana uwezo wa kutenda mema.
6 Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee BWANA; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza.