11 Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema BWANA; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.
12 Basi utawaambia neno hili, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila chupa itajazwa divai; nao watakuambia, Je, sisi hatujui ya kuwa kila chupa itajazwa divai?
13 Ndipo utakapowaambia, BWANA asema hivi, Tazama, nitawajaza ulevi wenyeji wote wa nchi hii, hata wafalme wanaoketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na makuhani, na manabii, na wenyeji wote wa Yerusalemu.
14 Nitawagonganisha, mtu na mwenzake, naam, baba za watu na watoto wao pamoja, asema BWANA; sitahurumia, wala sitaachilia, wala sitarehemu, hata nisiwaangamize.
15 Sikilizeni ninyi, kategeni masikio yenu; msifanye kiburi; maana BWANA amenena.
16 Mtukuzeni BWANA, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, na kabla miguu yenu haijakwaa juu ya milima yenye giza; na wakati mnapoitazamia nuru, kabla hajaigeuza kuwa kivuli cha mauti, na giza nene.
17 Bali kama hamtaki kusikia, roho yangu italia kwa siri, kwa sababu ya kiburi chenu; na jicho langu litalia sana na kutoka machozi mengi, kwa kuwa kundi la BWANA limechukuliwa hali ya kufungwa.