1 Neno la BWANA likanijia, kusema,
2 Enenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi,Nakukumbuka, hisani ya ujana wako,upendo wa wakati wa uposo wako;Jinsi ulivyonifuata huko jangwani,katika nchi isiyopandwa mbegu.
3 Israeli walikuwa utakatifu kwa BWANA;malimbuko ya uzao wake;Wote watakaomla watakuwa na hatia;uovu utawajilia; asema BWANA.
4 Lisikieni neno la BWANA, ninyi nyumba ya Yakobo, na ninyi, jamaa zote za nyumba ya Israeli.
5 BWANA asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili?
6 Wala hawakusema, Yuko wapi BWANA, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani, katika nchi ya ukame na mashimo, katika nchi ya kiu na ya kivuli cha mauti, katika nchi ambayo ndani yake hapiti mtu, wala haikukaliwa na watu?
7 Nami nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo.